5Mnafiki wewe! Ondoa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako na hapo ndipo utaona waziwazi kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilichoko jichoni mwa ndugu yako.
8Maana, aombaye hupewa, atafutaye hupata, na abishaye hufunguliwa.
9Je, kuna yeyote miongoni mwenu ambaye mtoto wake akimwomba mkate, atampa jiwe?
10Au je, akimwomba samaki, atampa nyoka?
11Kama basi ninyi, ingawa ni waovu, mwajua kuwapa watoto wenu vitu vizuri, hakika Baba yenu wa mbinguni atafanya zaidi: atawapa mema wale wanaomwomba.
12"Watendeeni wengine yale mnayotaka wao wawatendee ninyi. Hii ndiyo maana ya Sheria ya Mose na mafundisho ya manabii.
13"Ingieni kwa kupitia mlango mwembamba. Kwa maana njia inayoongoza kwenye maangamizi ni pana, na mlango wa kuingilia humo ni mpana; waendao njia hiyo ni wengi.
14Lakini njia inayoongoza kwenye uzima ni nyembamba, na mlango wa kuingilia humo ni mwembamba; ni watu wachache tu wanaoweza kuigundua njia hiyo.
15"Jihadharini na manabii wa uongo. Wao huja kwenu wakionekana kama kondoo kwa nje, lakini kwa ndani ni mbwa mwitu wakali.
16Mtawatambua kwa matendo yao. Je, watu huchuma zabibu katika miti ya miiba, au tini katika mbigili? La!