1Mimi Paulo, Silwano na Timotheo tunawaandikia ninyi jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambao ni watu wake Mungu Baba yetu na wa Bwana Yesu Kristo.
2Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
3Ndugu, tunapaswa kushukuru Mungu daima kwa ajili yenu. Inafaa kwetu kufanya hivyo kwani imani yenu inakua sana na kupendana kwenu kunaongezeka sana.
4Ndio maana sisi tunajivunia ninyi katika makanisa ya Mungu. Tunaona fahari juu ya jinsi mnavyoendelea kuamini na kustahimili katika udhalimu wote na mateso mnayopata.
5Hayo yote yanathibitisha kwamba hukumu ya Mungu ni ya haki, na matokeo yake ninyi mtastahili Utawala wake ambao kwa ajili yake mnateseka.
6Mungu atafanya jambo la haki: atawalipa mateso wale wanaowatesa ninyi,
7na kuwapeni nafuu ninyi mnaoteseka, na sisi pia. Atafanya jambo hilo wakati Bwana atakapotokea kutoka mbinguni pamoja na malaika wake na wakuu
8na miali ya moto, kuwaadhibu wale wanaomkataa Mungu na wale wasiotii Habari Njema ya Bwana wetu Yesu.
9Adhabu yao itakuwa kuangamizwa milele na kutengwa mbali na utukufu wake mkuu,
10wakati atakapokuja Siku ile kupokea utukufu kutoka kwa watu wake na heshima kutoka kwa wote wanaoamini. Ninyi pia mtakuwa miongoni mwao, kwani mmeuamini ule ujumbe tuliowaletea.
11Ndiyo maana tunawaombeeni daima. Tunamwomba Mungu wetu awawezeshe muyastahili maisha aliyowaitia myaishi. Tunamwomba, kwa uwezo wake, atimize nia yenu ya kutenda mema na kukamilisha kazi yenu ya imani.
12Kwa namna hiyo, jina la Bwana wetu Yesu litapata utukufu kutoka kwenu, nanyi mtapata utukufu kutoka kwake kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.