1Mimi Paulo, ambaye Mungu alitaka niwe mtume wa Kristo Yesu ili niutangaze ule uzima tulioahidiwa katika kuungana na Kristo Yesu,
2nakuandikia wewe mwanangu mpenzi Timotheo. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba na Kristo Yesu Bwana wetu.
3Ninamshukuru Mungu ambaye ninamtumikia kwa dhamiri safi kama walivyofanya wazee wangu; namshukuru kila ninapokukumbuka daima katika sala zangu.
4Nakumbuka machozi yako na ninatamani usiku na mchana kukuona, ili nijazwe furaha.
5Naikumbuka imani yako ya kweli, imani aliyokuwa nayo nyanya yako Loisi, na pia mama yako Eunike. Nina hakika kwamba wewe pia unayo.
6Ndio maana nakukumbusha ukiweke motomoto kile kipaji ulichopewa na Mungu wakati nilipokuwekea mikono yangu.
7Kwa maana Mungu hakutupa Roho wa kutufanya tuwe waoga, bali alitupa Roho wa kutujalia nguvu, upendo na nidhamu.
8Basi, usione haya kumshuhudia Bwana wetu, wala usione haya kwa sababu yangu mimi niliye mfungwa kwa ajili yake. Lakini shiriki katika mateso kwa ajili ya Habari Njema, kadiri ya nguvu unazopewa na Mungu.
9Yeye alituokoa, akatuita tuwe watu wake yeye mwenyewe, si kwa sababu ya matendo yetu wenyewe bali kwa sababu ya kusudi lake na neema yake. Alitujalia neema hiyo katika Kristo Yesu kabla mwanzo wa nyakati;
10lakini sasa imefunuliwa kwetu kwa kuja kwake Mwokozi wetu Yesu Kristo. Yeye amekomesha nguvu za kifo, na kwa njia ya Habari Njema akadhihirisha uzima usio kufa.
11Mungu amenichagua mimi niwe mtume na mwalimu kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema,
12nami nateseka mambo haya kwa sababu hiyo. Lakini niko bado timamu kabisa kwani namjua yule niliyemwamini, tena nina hakika kwamba yeye aweza kukilinda salama kile alichonikabidhi, mpaka Siku ile.
13Shika kwa makini mafundisho yale ya kweli niliyokufundisha, na kubaki katika hiyo imani na huo upendo wetu katika kuungana na Kristo Yesu.
14Jambo lile bora ulilokabidhiwa lilinde kwa nguvu ya Roho Mtakatifu anayeishi ndani yetu.
15Kama unavyojua, watu wote mkoani Asia wameniacha, miongoni mwao wakiwa Fugelo na Hermogene.
16Bwana aihurumie jamaa ya Onesiforo, kwa sababu aliniburudisha rohoni mara nyingi, wala hakuona haya kwa kuwa nilikuwa kifungoni,
17ila mara tu alipofika Roma, alianza kunitafuta kwa bidii mpaka akanipata.
18Bwana amjalie huruma katika Siku ile! Nawe wajua vizuri mengi aliyonifanyia huko Efeso.