1Mimi Paulo, Silwano na Timotheo tunawaandikia ninyi jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambao ni watu wake Mungu Baba, na wa Bwana Yesu Kristo.
2Tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu ninyi nyote na kuwakumbukeni daima katika sala zetu.
3Maana, mbele ya Mungu Baba yetu, twakumbuka jinsi mnavyoonyesha imani yenu kwa matendo, jinsi upendo wenu unavyowawezesha kufanya kazi kwa bidii, na jinsi tumaini lenu katika Bwana wetu Yesu Kristo lilivyo thabiti.
4Ndugu, twajua kwamba Mungu anawapenda na kwamba amewateua muwe watu wake,
5maana wakati tulipowahubirieni ile Habari Njema haikuwa kwa maneno tu, bali pia kwa nguvu na kwa Roho Mtakatifu, tukiwa na hakika kwamba ujumbe huo ulikuwa wa kweli. Mnajua jinsi tulivyoishi pamoja nanyi; tuliishi kwa manufaa yenu.
6Ninyi mlifuata mfano wetu, na kumwiga Bwana. Ingawa mliteswa sana, mliupokea ujumbe huo kwa furaha itokayo kwa Roho Mtakatifu.
7Kwa hiyo ninyi mmekuwa mfano mzuri kwa waumini wote wa Makedonia na Akaya.
8Maana, kutokana na bidii yenu ujumbe wa Bwana umesikika si tu huko Makedonia na Akaya, bali imani yenu kwa Mungu imeenea popote. Tena hatuhitaji kusema zaidi.
9Watu hao wanazungumza juu ya ziara yetu kwenu: jinsi mlivyotukaribisha, jinsi mlivyoziacha sanamu mkamgeukia Mungu aliye hai na wa kweli,
10na sasa mwamngojea Mwanae ashuke kutoka mbinguni, Yesu, ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu, na ambaye anatuokoa katika ghadhabu ya Mungu inayokuja.