1Mimi Paulo, mtume wa Yesu Kristo kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu na Yesu Kristo tumaini letu,
2nakuandikia Timotheo mwanangu halisi katika imani. Nakutakia neema, huruma na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Kristo Yesu Bwana wetu.
3Napenda ukae huko Efeso, kama nilivyokuomba nilipokuwa ninakwenda Makedonia. Wako watu fulani huko wanaofundisha mafundisho ya uongo. Wakomeshe watu hao.
4Waambie waachane na zile hadithi tupu na orodha ndefu za mababu, ambazo huleta tu ubishi, wala haviwajengi watu katika mpango ujulikanao kwa imani.
5Shabaha ya amri hii ni kuhimiza mapendo yatokayo katika moyo safi, dhamiri njema, na imani ya kweli.
6Watu wengine wamepotoka na kugeukia majadiliano yasiyo na maana.
7Wanapenda kuwa walimu wa Sheria, lakini hawaelewi maneno yao wenyewe au mambo wanayosisitiza.
8Twajua kwamba Sheria ni njema, kama ikitumiwa ipasavyo.
9Lakini tunapaswa kukumbuka kwamba sheria haziwekwi kwa ajili ya watu wema, bali kwa ajili ya wahalifu na wasiotii, wasiomcha Mungu na wenye dhambi, watu wasio na dini na wa kidunia. Watu wanaowaua baba na mama zao, au wauaji wowote wale;
10sheria imewekwa kwa ajili ya waasherati, wafiraji, wanaowaiba watu, waongo, na wanaoapa uongo au wanaofanya chochote ambacho ni kinyume cha mafundisho ya kweli.
11Mafundisho hayo hupatikana katika Habari Njema ambayo mimi nimekabidhiwa niihubiri, Habari Njema ya Mungu mtukufu na mwenye heri.
12Namshukuru Bwana wetu Yesu Kristo aliyenipa nguvu kwa ajili ya kazi yangu. Namshukuru kwa kuniona mimi kuwa ni mwaminifu, akaniteua nimtumikie,
13ingawa pale awali mimi nilimtukana na kumtesa na kumdhulumu. Lakini Mungu alinionea huruma, kwa sababu sikuwa na imani bado, na hivyo sikujua nilichokuwa ninafanya.
14Lakini Bwana wetu alinijalia neema yake kwa wingi, akanipa imani na upendo katika kuungana na Kristo Yesu.
15Usemi huu ni wa kuaminika, na tena unafaa kukubaliwa kabisa: Kristo Yesu alikuja ulimwenguni kuwaokoa wenye dhambi. Nami ni mkosefu zaidi kuliko hao wote,
16lakini Mungu alinionea huruma, ili Kristo aonyeshe uvumilivu wake wote kwangu mimi, kama mfano kwa wale wote ambao baadaye watamwamini na kupokea uzima wa milele.
17Kwake yeye aliye Mfalme wa milele na asiyekufa, yeye aliye Mungu pekee--kwake viwe heshima na utukufu milele na milele! Amina.
18Mwanangu Timotheo, nakukabidhi amri hii kufuatana na maneno ya unabii yaliyosemwa zamani juu yako. Yatumie maneno hayo yawe silaha yako katika kupigana vita vizuri,
19na ushike imani yako na dhamiri njema. Watu wengine hawakusikiliza dhamiri zao na hivyo wakaiharibu imani yao.
20Miongoni mwao ni Humenayo na Aleksanda ambao nimewakabidhi kwa Shetani, ili wafundishwe wasimtukane Mungu.